Masuala 10 yanayoweza kuzua mizozo katika ndoa
Wachumba wakikumbatiana. Picha/MAKTABA
Kwa Mukhtasari
NDOA ni
mojawapo ya hatua anazozipitia binadamu maishani mwake. Hata hivyo,
nyingi ya ndoa za siku hizi hazidumu kamwe. Inatamausha kuona kuwa,
baadhi yazo, hazidumu hata kwa muda wa miaka miwili tangu kuasisiwa
kwazo kutokana na mizozo na migogoro. PETER CHANGTOEK aliomba ushauri
kutoka kwa wawili waliofanikiwa:
NDOA ni mojawapo ya hatua anazozipitia
binadamu maishani mwake. Yamkini ni mkataba unaostahili kustahimiliwa na
wale waliofunga pingu za maisha.
Hata hivyo, nyingi ya ndoa za siku
hizi hazidumu kamwe. Inatamausha kuona kuwa, baadhi yazo, hazidumu hata
kwa muda wa miaka miwili tangu kuasisiwa kwazo.
Mojawapo ya sababu za kuvunjika kwa ndoa ni migogoro inayoshuhudiwa kila uchao katika familia nyingi.
Ili kuweza kuikabili migogoro hiyo, ni jambo bora kuvitambua vyanzo vya migogoro yenyewe.
Kasisi Leonard Kirui na mkewe Helen
Kirui, ambao ni washauri wa ndoa humu jijini Nairobi, na ambao ndoa yao
imedumu kwa miaka kumi na mitatu, wanasema kuwa, mingi ya migogoro hiyo
huanza wakati wa kuweka msingi ndoa zenyewe.
1. Kufichana mambo fulani
"Mingi ya migogoro hukita mizizi
iwapo mmoja kati ya wale waliooana hakumwambia mwenzake ukweli kabla
hawajaoana, halafu ukweli wenyewe ubainike baadaye, migogoro hiyo
huchipuka," anafichua kasisi huyo wa kanisa la The Living Light.
2. Pesa
Iwapo wawili waliooana kwa sababu ya
fedha, migongano kati ya wawili hao huenda ikose kuepukika. Bila shaka,
pindi tu fedha hizo ziishapo, migogoro hiyo hushuhudiwa.
3. Kazi
Hali kadhalika, amali au kazi pia huchangia baadhi ya migogoro inayoshuhudiwa katika nyingi za familia.
"Kama mmoja wa wawili hao hufanya
kazi mbali na nyumbani na hufika nyumbani akiwa amechelewa, au hata
kumaliza muda mrefu bila kuenda nyumbani, huenda mwanandoa mwenzake
akamtafuta rafiki wa nje ya ndoa, ili kuiridhisha nafsi yake kimapenzi,"
akaongeza kasisi huyo, ambaye pia ni mhubiri wa kimataifa.
4. Marafiki
Marafiki wasiofaa pia huchangia kuwepo kwa migogoro ya kila mara kwenye ndoa.
"Nafsi ya tatu haifai kupewa nafasi
kuyaingilia maswala ya wawili waliooana. Wanaweza kuruhusiwa tu kutoa
ushauri, bali si kutoa uamuzi kwao," akaongezea Bi Helen Kirui, ambaye
hujitolea kuwapa ushauri wanawake kuhusu maswala ya ndoa.
5. Elimu
Elimu, vile vile, imetajwa na
washauri hao kuwa kimojawapo cha viini vya migogoro inayotishia
kuziyeyusha na kuzisambaratisha ndoa nyingi. Wanadokeza kuwa, endapo
lipo pengo kubwa la kielimu kati ya wawili waliooana, ni dhahiri shahiri
kuwa migogoro itashuhudiwa. Wanasema kuwa, yule mwenye elimu ya juu
zaidi kuliko mwenzake huenda akajioana mwenye usemi mkubwa zaidi, hivyo
basi kumkera mwenzio.
6. Rasilmali
Isitoshe, rasilimali pia huchangia
kuwepo kwa migogoro mingi katika familia. Kuwepo au kutokuwepo kwa
rasilimali hizo kunachangia mno migongano hiyo ya kila mara. Zikikosa ni
mnung’uniko, zikitumiwa vibaya, pia ni migogoro.
7. Kutowajibika
Fauka ya hayo, kutowajibika
ipasavyo, kwa mujibu wa washauri hao wa ndoa, huchangia pakubwa kuwapo
kwa migogoro kwenye familia zisizohesabika.
"Mizozo hutokea iwapo mume hawi kiongozi. Ni lazima awajibike na awe mwenye maono," akafichua Bwana Kirui.
"Wake kwa maumbile yao wanafaa kuongozwa. Wao ndio hutoa maoni, na waume wao ndio hutoa uamuzi," akaongezea Bi Helen Kirui.
8. Dawa za kulevya
Vile vile, washauri hao wa ndoa
wanadokeza kuwa, migongano pia huchangiwa na matumizi ya dawa za
kulevya. Hakika dawa za kulevya zimetikisatikisa ndoa nyingi kama
Tsunami.
9. Pengo la kiumri
Hali kadhalika, pengo kubwa la kiumri lililoko baina ya wale waliooana huchangia kuwapo kwa migogoro katika familia nyingi mno.
"Ikiwa wale wanaooana wana tofauti
kubwa wa kiumri, yaani kama miaka 14 hivi, au zaidi, watakuwa wakizozana
kwa sababu labda mwengine ambaye ni mdogo atakuwa na hisia nyingi, na
labda yule mwengine hanazo," anafichua kasisi huyo.
10. Watoto
Aidha, kukosa kuzaa watoto pia
huchangia kushuhudiwa kwa migogoro katika ndoa nyingi, kwa mujibu wa
washauri hao wa ndoa. Wanasema siyo tu kukosa kuzaa watoto ndiko
kunachangia migogoro hiyo, bali pia kuzaa watoto wa jinsia moja.
Suluhisho liko wapi?
ILI kukabiliana na migogoro hiyo, ni
jambo aula kwa wale wanaonuia kufunga nikahi kuwa na uwazi na kuambiana
ukweli ili kujua iwapo watavumiliana watakapooana.
Hali kadhalika, ni bora kwao
kuvitembelea vituo vitoavyo ushauri na nasaha kuhusu maswala ya ndoa.
Vile vile, kusiwe na pengo kubwa la kiumri na kielimu.
Pia, kila mmoja anastahili
kuwajibika ipasavyo, ili kuzuia kuchipuka kwa migogoro hiyo. Ikiwa mtu
mmoja anafahamu fika kwamba amefanya makosa, anastahili kuwajibika na
kurekebisha mambo. Jamii ikikumbwa na matatizo fulani, mzee mwenye
nyumba anafaa kuingilia kati na kuleta suluhu.
Aidha, rasilimali zilizopo sharti
zitumike ipasavyo, zisitumiwe kwa ubadhirifu. Isiwe kwamba mmoja katika
ndoa ndiye anayeonekana kufurahia mali pekee huku mwingine akihisi
kutengwa. Kwa mfano, ikiwa baba ana mali nyingi, lakini hatoi kiasi
kizuri cha pesa za matumizi mle nyumbani na badala yake kufurahia na
wenzake kule nje, bila shaka jambo hili litazua sintofahamu.
Kukosa kujaliwa watoto
Na kuhusu kukosa kuzaa watoto,
washauri hao wanawashauri wahusika kuutafuta usaidizi wa daktari. Kwa
sababu huenda yule anayemlaumu mwenzake akawa ndiye mwenye tatizo.
Aidha, kumekuwa na maendeleo mengi ya kisayansi ambayo yanaweza kusaidia
wanandoa kupata mtoto.
Pia, washauri wanaonya dhidi ya
kuweka thamani sana kwenye watoto wakisema kwamba wawili wanaweza kuwa
na furaha kubwa hata bila kuwa na watoto. Kadhalika, wanasema kwamba
kuna mbinu nyingine za kupata watoto ikiwemo kupanga kutoka kwa makao ya
watoto.
Lakini la muhimu mno, ni vyema kwa
wawili kuketi chini na kutathmini viini ya migogoro hiyo, na kuwasiliana
jinsi ya kuikabili. Iwapo watajua viini vya migogoro hiyo, bila shaka,
suluhu zitapatikana. Na hivyo basi, kuipunguza au kuimaliza kabisa
migogoro yenyewe.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni