Jumapili, 5 Machi 2017

Assalaam alaykum Warahamtullahi Wabarakatuh.
Misingi au njia ya kuamiliana na watu, tunayapata katika wasia wa Allah uliokuja katika Qur'an ndani ya Surat Alhujurat, uzingatieni.
1⃣ unapoletewa khabari yoyote basi kwanza unatakiwa uichunguze kwanza ili ujue uhakika na ukweli wake, ili usije kulihukumu jambo kimakosa ukaja ukajuta baadae, hali ya kuwa majuto yatakuwa mjukuu muda huo.
2⃣ Pindi ukitokea ugomvi baina ya Waislamu wawili, au makundi mawili, Basi Allah mtukufu anatuusia kusuluhishana na kupatanishana, kwa kutumia kila njia ya kidiplomasia kufikia lengo, na si kukaa kufurahia na kuchochea ugomvi, hii si tabia ya Muumini.
3⃣ Pia Allah mtukufu anatuusia kuwa waadilifu na kutenda haki tunapotoa hukumu, na si kumpa haki mmoja na kumdhulumu mwengine.
NB: Haki na uadilifu unaingia pia katika Mizani hasa katika nyanja za Biashara, wauzaji wawe waadilifu na wajitahidi kadri wanavyoweza kutowadhumu wateja wanapowapimia bidhaa.
Na wale wahusika wa Mizani katika ofisi za kununua Karafuu, Mwani, Pamba nk, wawe waadilifu na watenda haki katika Mizani, Allah ametoa onyo kali juu ya hili.
4⃣ Allah mtukufu pia anatuusia kuhusu suala zima la kutofanyiana mizaha mikubwa na suala zima la kudharauliana na kubaguana, kwani huwenda huyo unayemdharau akawa ni bora mbele ya Allah mtukufu, hata akawa maskini,mnyonge, dhaifu, kabila yake si tukufu/kubwa, rangi yake,cheo chake na mambo yanayofanana na hayo, wanaadamu sote ni sawa tofauti za kimaumbile tulizonazo ni mwenyewe Allah andiye aliyetaka hivyo, na hii yote ni kuonesha uwezo wake na fani yake katika kuumba.
5⃣ Allah pia anatuusia kutovunjiana heshima, sisi sote ni wakarimu Allah ametutukuza na kutufanya kuwa viumbe bora kuliko wengine ulimwenguni, kwa hivyo kila mmoja anatakiwa kumuheshimu mwenzake na kuheshimu mawazo na maamuzi yake.
6⃣ Allah mtukufu anatuusia kuacha kuitana kwa majina mabaya na kuchokozana, hiyo ni tabia ya watu mafasiki, sisi Waumini haifai kufanya hivyo, tuitane kwa majina yaliyo mazuri, yenye maana nzuri, yanafurahisha mioyo yetu, na wasia huu pia kwa wazazi Allah anapowaruzuku watoto wawape watoto wao majina mazuri kama majina ya Masahaba na mitume na watu wema.
7⃣ Allah mtukufu anatuusia tuache tabia ya kudhaniana vibaya, kwani hakika ya dhana ni uovu/dhambi, tunatakiwa siku zote tuwe na dhana nzuri kwa wenzetu huo ndio uislamu.
8⃣ Pia Allah mtukufu anatuasa kuacha tabia ya kuchunguzana, kufuatiliana na kupelelezana, si tabia nzuri kuchunguza aibu za mwenzako, na muislam aliye bora ni yule anayejiweka mbali na mambo yasiomuhusu, kufanya hivyo ni kujiweka mbali na matatizo.
9⃣ Allah mtukufu anatuusia pia kuacha tabia ya kusemana vibaya nyuma ya pazia na kusengenyana, kufanya hivyo ni sawa na kula nyama ya ndugu yako unayemsengenya anapokuwa maiti.
Haya yote Allah mtukufu anatuusia kuachana nayo, kufanya hivyo ndio tutasalimika hapa duniani kwa kuishi maisha ya furaha na kusalimika huko Akhera tunakokwenda.
Tafadhali watumie na wengine nao waujue wasia wa Allah uliokuja ndani ya Surat Alhujurat.
Kama kuna kosa rekebisha, Allah anajua zaidi.
Abuu Zahrah Masoud Al-Bimani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni