Jumapili, 5 Machi 2017


DONDOO ZA MUHIMU KATIKA NDOA!
Nina kila sababu ya kumshukuru Muumba wangu kwakuwa ni yeye ndiye mlinzi na kiongozi wa maisha yangu, naamini bila yeye mimi na wewe tusingekuwepo hivyo basi tuna wajibu wa kumshukuru kila wakati. bila shaka kwa nguvu zake yeye aliye juu utakuwa mzima wa sifa njema na macho na akili yako vimejiandaa kupata darasa hili murua la maisha.
Leo nitazungumza moja kwa moja na wanandoa. Nitazungumza juu ya jambo muhimu sana, nazungumzia unyenyekevu na uvumilivu katika ndoa bila kujali jinsia, je ni utumwa? Hapa kila mmoja atakuwa na jibu lake, lakini leo nataka kuwapa ukweli wa kitaalamu. Kuna usemi usemao ukitaka kujua uhondo wa ngoma uingie ucheze, wengine pia husema ukitaka kujua utamu na uchungu wa ndoa basi uwe mwanandoa, usemi huu una kweli ndani yake, wewe ambaye hujaingia kwenye ndoa naamini si rahisi kujua shida ama starehe apatazo mume ama mke ndani ya ndoa, pengine kama utazijua ni kwa kuzisikia kwa wanandoa ambao wanaeleza maisha yao. Hata kama utayasikia hutajua ukweli yampatayo mwenzio mpaka yakukute mwenyewe kwani mengi huwa ya siri za ndoa.
Kuna matatizo mengi wapatayo wanandoa, ukiniambia nitaje matatizo yaliyopo katika ndoa za watu nitaeleza mengi sana kutokana na uzoefu wangu pamoja na tafiti mbalimbali zilizofanywa na wataalamu wa mambo ya mapenzi.
Lakini wakati nikizitaja kero za ndoa pia kuna upande wa pili ambao ni furaha, pia kuna mengi mazuri wayapatayo wanandoa wanakuwa katika ndoa zao.
MAANA YA NDOA
Ndoa ina maana kubwa sana katika maisha ya binadamu, hata hivyo ina tafsiri nyingi kulingana na imani au mahali ndoa ilipofungwa! Kwa Wanasaikolojia ya Mapenzi ndoa ni ukamilifu wa makubaliano ya muungano wa mwanamke na mwanaume wenye kupendana kwa lengo la kuishi pamoja kama mume na mke kulingana na sheria ya dini, mila au desturi za sehemu fulani.
Pamoja na tafsiri hiyo ambayo hutambuliwa na wataalamu wa mambo ya mapenzi, hawashauri wanandoa kuachana, maana kama waliungana kwa upendo basi wan apaswa kuishi kwa upendo na kusikilizana siku zote, huo ndiyo upendo wa kweli ambao Wanasaikolojia wa Mapenzi wanatambua.
ULINZI WA NDOA
Hapa ndipo kwenye msingi wa mada yetu, unapoingia kwenye ndoa kitu cha kwanza unatakiwa kufikiria jinsi ya kuilinda ndoa hiyo kwa gharama yoyote! Kuingia kwenye ndoa na kutoka baada ya muda mfupi ni kujitafutia laana ambayo haina ulazima wowote, hapa unatakiwa kufikiria mpaka mwisho wa uwezo wa kufikiri ili ndoa yako idumu na usije ukajikuta umeingia katika laana hiyo.
Linapokuja sasa suala la ulinzi wa ndoa yako, utashindwa kumnyenyekea mpenzi wako? Unatashindwa kumvumilia mpenzi wako kwa sababu utajihisi wewe ni mtumwa wa mapenzi? Wapi imeandikwa hii? Mathalani mkeo anaumwa na kwa bahati mbaya hamna msichana wa kazi, je utashindwa kumsaidia kazi kama kupika, kufua, kuosha vyombo na kazi nyinginezo kwasababu tu, wewe ni mwananume? Haingii akilini hata kidogo.


UVUMILIVU...
Katika maisha anayohitaji kuyavumilia mwanadamu ni maisha ya ndoa. Ndoa inakuwa na mambo mengi sana, kutunza familia, kupeana haki za nyumba, kusaidiana na kuvumiliana katika vipindi vya dhiki na faraja na mengineyo. Ukarimu, uaminifu, upendo wa kweli ni kati ya chachu za kudumisha penzi na kamwe halitaweza kuchuja.
Unapooa au kuolewa lazima ufahamu kuwa unakuwa umejenga undugu baina ya familia yako na ya mwenzio. Katika kuishi kwenu huko utakutana na matabaka mengi, watu hutofautiana tabia, mfano wewe mwanamke umeolewa, mumeo akaleta ndugu, yaani wifi zako.Unatakiwa kuwasoma wifi zako tabia ili uweze kuendana nao, ili kufanikiwa unapaswa uwe na busara, mvumilivu, mnyenyekevu, na kuonyesha kuwajali, hii inaweza kukusaidia sana kwani watakapokutendea mambo ya ajabu nawe ukaanza kuwaropokea matusi, utakuwa unajingiza kwenye migogoro ambayo mwisho wake huweza kuwa mbaya zaidi kwako kuliko kwao.
Kumbuka kuwa Mungu ametuumba kila mtu na udhaifu wake, ndio maana unaona wanandoa wengi wanajikuta wakizikimbia ndoa zao kwa kutendwa na wandani ama ndugu wa wandani wao, wakati mwingine mume anaweza kuwa hajui, unayepaswa kumweleza ni wewe, na unapomweleza lazima uzingatie heshima na busara ambayo haitaonyesha kwamba umedharau ukoo wao.
Sio unaanza kusema; "Nyoo! Umeniletea ukoo wenu hapa, chakula hakitoshi! Nitawafukuza!" Kwa kauli hiyo utaonekana limbukeni, kaa naye chini zungumza naye kwa ukarimu mweleze ni jambo gani linalokunyima uhuru wewe kama mkewe wa ndoa. Usimfiche, mwambie; "Mume wangu, kuna jambo wifi amenitendea sijui kama anaona ni kosa lakini mie naona amenikosea, mweleze asirudie tena," tena hakikisha wakati unamweleza haya mpo peke yenu chumbani na huenda ni baada ya kumpa haki yake. Upo hapo?
Huo ndiyo uvumilivu ninaouzungumzia, siku zote wewe ndiye unayetakiwa kuwa na uchungu na ndoa yako. Kabla ya kuzungumza jambo lolote fikiria mara mbili, halitasababisha matatizo kwako? Ukipata matatizo au kuachika huyo wifi yako atakuwepo? Jibu ni hapana! Utakaporudishwa nyumbani kwenu, utawaangaliaje wazazi wako ambao walikulea katika malezi mazuri na kukufunda vyema? Ni nini kama siyo aibu mtoto wa kike utakuwa umewapelekea wazee wako?
Kaa chini, fikiria kwa makini kabla ya kuamua jambo lolote linalohisu ndoa yako. Kumbuka kuwa kuingia kwenye ndoa ni kazi ngumu lakini kazi ngumu zaidi ni kuhakikisha unailinda ndoa yako inaendelea kuwa hai siku zote, ndiyo kusema kwamba siku mnasherehekea miaka 10 au jubilee ya ndoa yenu utakuwa ukijimiminia misifa kibao kibao kuwa kama siyo uvumilivu wako usingeweza kufikia hatua hiyo.
UNYENYEKEVU JE?
Sawa kabisa! Sasa kama usipomnyenyekea lahazizi wako, ambaye mwenyewe ulikubali kuwa naye na kufunga naye ndoa unataka umnyenyekee nani? Mumeo/mkeo ndiyo wa kumnyenyekea siku zote za uhai wako. Lazima uwe na kauli ya upo iliyojaa ukaribu. Ndoa kubembelezana bwana, mpenzio akija na mawazo yake, mtu amemuudhi kazini kwako ndio mahali haswa anapopaswa kunyenyekewa na kupewa raha.
Wewe ndiye unapaswa kumsahaulisha kabisa mambo yote yaliyotokea kazini. Mpokee kwa upole, mwambie poile, mkaribishe chumbani kisha mvue nguo zake na umpeleke bafuni mwenyewe. Anza kumwogesha bila kuzungumza naye maneno mengi. Tumia dodoki au kitambaa laini kumsafisha ngozi ya mwili wake.
Baada ya hapo mkaushe kwa taulo laini kisha mrudishe chumbani, mtolee nguo za usiku kisha mpeleke mezani kwa chakula. Baada ya hapo sasa mkiwa sebuleni mnaangalia tamthiliya mwulize kwa upole huku macho yakiwa yanazungumzia mapenzi. “Darling vipi, mbona leo naona sio kawaida yako? Umechokachoka...kuna nini mpenzi wangu jamani?” Amini nakuambia kwa kauli kama hiyo hata kama alikuwa na tatizo kubwa anaweza akakujibu; “Ah kuna mtu aliniudhi kidogo ofisini, lakini baada ya kufika hapa nyumbani najisikia amani sasa,” tena wakati anakuambia hivi ujue lazima atakuwa anaachia tabasamu mwanana sana.
Nikufundishe tena hapo cha kufanya? Mh! Unamsogelea kisha unabusu halafu unapima joto la homa yake ya mapenzi, kama limepanda mshike mkono mwahishe chumba cha upasuaji kabla hujampoteza mtoto wa mwanamke mwenzio.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni