Jumapili, 5 Machi 2017

Ktk ndoa, hupati yote, wala hukosi yote !
Watu wengi kabla hawajaingia kwenye jambo la ndoa, huwa na mitazamo yao kuhusu ndoa yenyewe. Lkn uzoefu unaonesha kuwa, wakishaingia kwenye ndoa, sehemu kubwa ya mitazamo yao kuhusu ndoa inabadilika. Moja ambalo ni la ukweli na haliwezi kupingika ktk ndoa ni kuwa, kwenye ndoa hupati yote, wala hukosi yote.
Kwa sababu ndoa ni maisha ya watu wawili waliozaliwa tofauti na aghlabu wamekulia kwenye mazingira tofauti -- muhanga unaowakabili mbele yao ni kwenda kuanzisha jambo jipya ambalo hawajawahi kuwa na uzoefu nalo. Huenda jambo hilo likawafanya waache baadhi ya waliokuwa wameyazoea na kupokea baadhi ya ambayo hawakuwa wameyazoea.
Kuna baadhi ya watu kwenye familia walizotoka wamezoea kuwa na sauti, lkn wakifika kwenye ndoa huenda wakakutana na mazingira wakalazimika kuwa mabubu. Na kinyume chake, kuna watu waliozoea ktk familia zao kuwa mabubu, huenda ktk ndoa watakazoziingia wakalazimika kuwa na sauti. Wengine wanatoka kuwa wakali na kulazimika ndani ya ndoa kuwa wapole. Wengine wanatoka kuwa wapole, na kulazimika kuwa wakali. Wengine wanatoka na majivuno/kiburi/kujikweza, wakifika ndani ya ndoa wanashuka Na kinyume chake. Wengine ni watu wa kukataa kila kitu, wakifika kwenye ndoa inabidi wakubali kama si kila kitu walau basi baadhi ya vitu. Na wako waliozoea kukubali kila kitu, wakifika kwenye ndoa huenda wakalazimika kukataa kila kitu au baadhi ya vitu. Kwa muhtasari, ndoa ni hatua kubwa ya mapinduzi ktk maisha ya mtu binafsi. Ndoa inampindua mtu kutoka alivyokuwa kwenda asivyokuwa mwanzo.
Jambo muhimu hutegemea mtu na mawazo aliyonayo kabla ya ndoa kwamba anaitafsiri vp ndoa? Je, ndoa ni sehemu ya muhanga ktk maisha: kwamba viko vitu itakulazimu uvisamehe kwa ajili ya kulinda ndoa, au ndoa isamehe vitu kwa ajili ya kulinda fikra, mitazamo na mazoea yako? Yaani; ndoa ni kitu kikubwa zaidi kuliko maisha uliyokuwa nayo kwa maana kuwa maisha uliyokuwa nayo unaweza kuyaacha au maisha ulokuwa nayo ni muhimu zaidi kuliko ndoa, na kwa hivyo ndoa lazima ifuate maisha ulokuwa nayo? Ktk falsafa hio nzito, ndipo unapoona tajiri akamuoa maskini, maskini akaolewa na tajiri, mlemavu akaolewa na asiekuwa mlemavu nk.
Kati ya yote hayo, lo lote linaweza kutokea: alikuwa tajiri kabla ya ndoa, baada ya ndoa akawa maskini. Au mtu kuwa mzima kabla ya ndoa; na baada ya ndoa akawa mlemavu au mgonjwa na mfano wa hayo.
Mtu yo yote anaedhani kuwa inaweza kuwepo ndoa isiyokuwa na matatizo basi anajidanganya. Ukisikia ndoa fulani haina matatizo maana yake ni kuwa wavumilivu sana wanandoa hao. Hakuna manaa yo yote inaposemwa ndoa haina matatizo zaidi ya kuwa na maana ya kuvumilia. Ndoa zote zina matatizo. Kinachotofautiana inaweza kuwa ni aina ya matatizo. Mathalan, wengi wetu ni wenye kuendesha gari. Gari hizo haziwi na matatizo? Hazijawahi kutusumbua? Sasa ndio tusiendeshe gari kwa kuwa zinakuwa na matatizo au kwa kuwa zimewahi kutusumbua? La ! Hasha ! Ndio pale aliposema Kandoro ktk mashairi yake kuwa: "kuchafuka kwa Bahari, sio mwisho wa safari". Yaani, kwa kuwa Bahari imechafuka, sisafiri tena ! Bahari kuchafuka ndio twabia yake. Meli iko salama bandarini; lkn kutengenezwa kwake hakukuwa kwa madhumuni hayo (ya kukaa bandarini).
Neno taasisi linamaanisha mkusanyiko wa watu tofauti ndani ya aina moja ya maisha. Ikiwa hivyo ndivyo, basi hakuna taasisi muhimu zaidi kuliko taasisi ya ndoa kwa sababu inawakusanya watu wawili tofauti, wenye kutoka mazingira tofauti, twabia tofauti, mitazamo tofauti kwa shabaha ya kuwaweka pamoja milele. Na kwa kuwa msingi mkubwa wa watu kuishi pamoja ni kuvumiliana -- basi hakuna siri ya mafanikio kwa taasisi yo yote ile isipokuwa kuvumiliana. Na ni kwa uvumilivu tu ndio maana ndoa za baadhi ya maskini zinadumu na za baadhi ya matajiri zinavunjika kwa kukosekana uvumilivu. Umasikini na utajiri sio unaoamua kuwa ndoa idumu au isidumu. Au mathalan nani asiekosea? Tunakubaliana kuwa makosa yanatofautiana kwa ukubwa na udogo; lkn makosa yapo kila upande. Siri ya mafanikio ktk ndoa ni uvumilivu. Wenye mke mmoja wana migogoro, wenye wake wengi wana migogoro. Wazinifu wana migogoro, wasokuwa wazinifu wana migogoro. Matajiri wana migogoro, maskini wana migogoro. Wasomi wana migogoro, wajinga wana migogoro kwenye jambo linaloitwa ndoa.
Uliza yo yote unaemuamini kwa uzoefu kuhusu siri ya ndoa - jibu lake lazima litakuwa UVUMILIVU

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni